AMSHA MOYO WA SIMBA NDANI YAKO.
Ikiwa ni miaka kadhaa tangu uwepo duniani umewahi jiuliza umewahi fanikisha mambo mangapi, Kama hujawahi Leo unaweza jifunza kitu kipya au Kama umefanikisha leo unaweza kuongeza kitu kwenye Ufahamu wako. Siri moja wapo ya kufanikisha kitu ni kuwa simba wa eneo linalokuzunguka, simba angurumaye kwa ujasiri na nguvu akiamini hakuna simba mwingine eneo analoishi au eneo la kazi anayoifanikisha. Simba akinguruma sauti yake husikika zaidi ya kilomita 8. Mara nyingi watu wamemtumia kuonesha nguvu na ujasiri katika kazi zao.
Simba sio mnyama mkubwa kuliko wote Wala Sio mwenye nguvu kuliko wote mwituni, lakini amepewa jina la kuitwa mfalme wa mwituni. Ukimfatilia kwa Karibu simba ni mnyama anayetumia muda mrefu kupumzika na kundi dogo la familia, kwajina lingine anaonekana kuwa ni mvivu sana. Simba awindaye mara zote huenda na mwenzake au wenzake wawili ila sio kwa pamoja bali ni kwa kunyata kwa ujanja mwingi.
Leo tujikite kujifunza tabia za mtu mwenye kufanikisha jambo kupitia kumfahamu simba wa mwituni. Fursa za kufanikiwa zipo nyingi ila zinahitaji umakini sana na kufahamu nidhamu ya kupata hiyo fursa na kula matunda yake. Simba anatuhamasisha leo ili tukamate fursa mikononi mwetu na kushinda.
Kujiongoza mwenyewe.
Simba hafuati kundi, anaishi kwenye kundi la ndugu wachache ila inapofika wakati wa kazi huinuka na wazo lake na kuanza kufanyia kazi bila kungoja kusukumwa. Mfuata kundi hajui anapokwenda hajui anachotakiwa kufanya Wala hajui nyakati za kufanya. Wakati mwingi mtu anayefuata kundi hiushia kuongozwa kwenye machinjio mfano wanyama wengi wanaotembea kimakundi huliwa. Sababu kubwa ya wao kuliwa ni kuongozwa na kiongozi asiyefaa kuwaongoza, asiyejua mahali pa kuwapeleka wala asiyejua nini wanataka. Kiongozi sahihi wa maisha yako ni wewe mwenyewe. Nimeshuhudia watoto yatima wengi wakiishia maisha ya kufanikisha malengo yao, sababu kubwa ni kuwa walikosa watu wa kuwaongoza na kujikuta wanajiongoza wao wenyewe kwakutumia Ushauri wanaopata kwa watu.
Ndani ya kila mmoja wetu Kuna moyo wa simba kazi kubwa ni kuamsha huo moyo na kuanza Kujiongoza mwenyewe Kama simba afanyavyo. Kuwa na ushujaa wa kusimama mwenyewe na kwenda uelekeo ambao hamna mtu anakwenda huko. Hata kama wengine wanaenda uelekeo mwingine wewe ukaamua kusonga mbele uelekeo wako mwenyewe. Wewe tu pekee unayejua kinachokufaa wewe tu pekee unayejua njia gani unaweza pita. Kama simba tumia hiyo mamlaka ya uongozi uliyonayo vizuri ili kukufanikisha.
Ufunuo wa Yohana 5 : 5
Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba.
Yesu kristo amefananishwa na simba kwasababu ya tabia yake ya uongozi, ameweza kufanya jambo ambalo walishindwa wengi na kuonekana Kama alijitolea si kwa moyo wa kibinadamu wa kuhesabu gharama ya maumivu bali ni kwa moyo wa simba. "Simba aliye wa kabila la Yuda" kwanini isiwe tembo? Simba anaweza kufanya mengi ambayo wengi hawawezi kufanya. Wamisri wanatumia ngozi na sanamu ya simba yenye sehemu ya kichwa Kama ishara ya utawala na mamlaka kwa Mfalme.
Kutumia nguvu na Ushujaa
Unajua unaweza fanya jambo kwa muda mchache na kulifanikisha Kama ukitumia nguvu zote ulizojaliwa kupewa na Mungu. Simba wa ukweli wanapata hasira ya kufanikiwa inapokuja wakati wa kufanya jambo. Kuwekeza muda mrefu kwenye jambo sio kipimo cha kufanikiwa bali kuwa na moyo wa kuwekeza nguvu zote yaani kutoacha mpaka ufanikiwe.
Siku moja nikifatilia makala ya wanyama pori nikajionea maajabu ya simba jike ambao ndio wawindaji kimajukumu, mara baada ya kujichagulia mnyama kwenye kundi ili amwendee hakumwacha mpaka alimpata licha ya kuumizwa sana. Wakati mwingine unaweza kuonekana kama king'ang'anizi wa jambo ama mbishi sana ila ndio namna ya kuchokoma kimaendeleo. Simba wa ukweli wanaonesha haswa wao ni nani wala hawatafuti heshima. Wanaamrisha heshima inawafuata wao. Simba anaitwa mfalme wa mwituni Kwani kuna kura iliwahi pigwa ndio akashinda? Jibu ni hapana bali anajipatia heshima kwasababu ya sifa zake.
Waamuzi 14 : 18
Nao watu wa mji wakamwambia siku ya saba kabla ya jua kuchwa,Ni kitu gani kilicho tamu kuliko asali? Ni kitu gani kilicho na nguvu kuliko simba? Naye akawaambia, kwamba hamkulima na mtamba wangu,Hamngekitambua kitendawili changu.
Hakuna kitu chenye nguvu kuzidi simba, ukiangalia umbo huwezi jua nguvu ya simba subiri wakati wa kazi ufike Utajua kuwa yeye ndiye Simba mfalme wa mwituni.
Kujua kulenga shabaha
Aliyewahi kuangalia tukio la simba anayekamata windo Utajua nini naongelea. Simba hutumia muda kuchagua windo lake tena hawi simba mmoja, wanajipanga kufuata windo lililonona kutoka mbali. Shabaha ya simba yeyote ni shingoni mahali damu itawezekana kunyonywa kwa wingi, sio ili simba ashibe damu bali mnyama aishiwe nguvu za kukimbia tena na huo ndio mwisho wa habari zake.
Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali Bwana huziongoza hatua zake.
Kila lengo lazima liwe mahususi, wazi, maalumu, linalopimika na lenye muda. Kazi yako ni kupanga na Mungu anaongoza mipango yako, kumtegemea Mungu hakufanyi hushindwe kupanga kisa unaimani sana. Mtu wa kawaida huwa na imani, matumaini na matarajio lakini mtu wa hali ya juu huandaa mipango na malengo kwa ujasiri.
Mtazamo chanya juu yako.
Licha ya kujibu maswali haya matatu ya: Unataka kufanya nini? Upo mahali gani( hali yako ya sasa) na utafikaje huko, inahitaji Mtazamo chanya ili kuweza kujibeba jinsi ulivyo maana kwa hali ya kawaida hali uliyonayo haifanani na vile Unataka kuwa. Mtazamo ni nini unafikiri, nini unafanya na nini unahisi juu yako, Mtazamo ni kila kitu kwenye maisha yako. Vyovyote vile ukiongezeka ama kushuka kimaendeleo ni kutokana na unavyojitazama wewe mwenyewe kwa wakati huo. Mtazamo wako unabashiri viwango vyako vyako kimaendeleo. Mtazamo wa kuendelea kusonga mbele wakati mbele kunazidi kuwa kugumu.
Nini Mtazamo wako kuhusu maisha? Unajiwazia nini?
Unajifiria Kama vile Mungu anavyokufikiria au unafikiri kama marafiki na ndugu wanavyokufikiria? Unahitaji Mtazamo wa simba, Mtazamo wa kuchukua hatamu na kusema ninaweza. Usiongee mawazo tembea mawazo yako.
Kutumia Ujasiri
Kuwa na nguvu ya kwenda mbele kwa akili kufuata uelekeo wako. Huwezi kuwa kiongozi kama huna uwezo wa kutumia ujasiri ulionao. Kiongozi mzuri ni yule aliyeweza Kutumia moyo wa simba ulio ndani yake. Kujiamini kwenda uelekeo wako ulioubuni mwenyewe na kuwa mvumbuzi wa mafanikio yako.
Mithali 28 : 1
Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba.
Maandiko bado yanamwelezeka simba kuwa anasifa ya ujasiri na ushujaa. Mioyo ndio hutushawishi kukimbia matatizo badala ya kupambana na matatizo.
Waefeso 3 : 12
Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini.
Imani pekee haitoshi kukufanya upate kile unachokitaka, mfano wa mama aliyetokwa damu kwa miaka kumi na miwili alikuwa na imani ya kuponywa lakini tofauti yake na wengine waliomzunguka Yesu ni ujasiri wa kutoka kwake na kumwendea Yesu licha ya kuwa alitambuliwa kuwa ni najisi.
Uamuzi.
Maisha yamejawa na vipindi vya kufanya maamuzi mapya kila siku na kutunza msimamo huo kwa muda fulani. Mtu anayemwamini Mungu anatakiwa kufanya maamuzi ya kumtegemea Mungu na kuweza kuomba kwa Mungu kile anachotaka lakini ukikosa maamuzi huwezi kuomba ipasavyo maana hutajua kitu cha kuombea. Maamuzi yatakupeleka kwenye mpango mkakati, ukikosa maamuzi utaishia kuwa na mipango mingi iliyokosa mikakati.
Mithali 30 : 29 -30
Kuna watatu wenye mwendo wa kupendeza, Naam, wanne walio na mwendo mzuri. Simba aliye hodari kupita wanyama wote; Wala hajiepushi na aliye yote;
Mwendo au mwenendo au tabia yake simba inatokana na maamuzi aliyojiwekea. Kama umewahi kuona makala ya simba au kumuona moja kwa moja unaweza kugundua kuwa simba kabla ya kufuata windo lake lazima awe amefanya maamuzi ya yupi haswa atamkamata. Simba hali kila anachokiona mbele yake bali anakula kile alichokipanga. Kwenye kundi la nyumbu wengi simba anafanya maamuzi ya nyumbu gani anamfaa kwa siku ile na uwe na uhakika huyo nyumbu analiwa siku hiyo. Akimkosa huyo atatulia kufanya maamuzi upya. Ukijipa muda wa maamuzi huwezi kukosa shabaha uliyonayo na ukikosa litakuwa darasa tosha kwako.
Mwisho kabisa tunaona kuwa bwana simba amejichukulia ufalme wa mwituni kwa urahisi kwasababu ya uwezo wake wa kudhihirisha kitu kilicho ndani yake. Siku zote fahamu kuwa hakuna kitu chepesi kufanya duniani yote ni magumu na yanahitaji moyo wa simba. Kila mtu ana moyo wa simba, kuwa Kama simba bila woga chimba barabara ya kuelekea mafanikio yako kwa nguvu zote nenda uelekeo wako. Simba sio wa kusitasita hana walakini au labda, anatimiza majukumu aliyonayo kwake na kwa jamii.
Mwanzo 49 : 8 - 9
Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia. Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakaye mwamsha?
Nahumu 2 : 12
Simba alirarua vipande vipande chakula cha kuwatosha watoto wake, aliwasongea wake zake nyama, aliyajaza mapango yake mateka, na makao yake aliyajaza mawindo.
AzimiaLeo🇹🇿
Comments