UNAWAZO GANI?
Mwanzo wa kila kilichowahi
kufanikiwa ni wazo, wazo lililobadilishwa na kuwa kitu halisi. Kabla hujawa na
wazo hilo unatakiwa kuwa na picha ya wapi unataka kufika au nini unataka
kufanya. Inakuwa bahati kama unapata mtu wa kukusaidia kuona picha yako kubwa
kuhusu maisha yako, vinginevyo unatakiwa uone mwenyewe hiyo picha na utengeneze
wazo la kukufikisha huko.
Katika ulimwengu huu tunaoishi mawazo yatakayosaidia makundi makubwa ya watu ndio yanayoweza kushinda na kuishi kwa Muda mrefu.
Wengi wanaoanzisha mawazo huanzia
kutoka kiwango cha chini na kuwa na mipango ya kupanda kuelekea juu hadi mawazo
yanapowapeleka. Lakini kikwazo kikubwa kwa hili ni kwamba wengi wanaoanzia
chini wanashindwa kuinua vichwa kuona FURSA zilizowazunguka kutokana na mawazo
waliyonayo kwahiyo wanabaki na mawazo mazuri wakiwa chini. Inatakiwa kukumbuka
kuwa mwonekano wa huko chini sio mzuri na unatabia ya kuua tamaa ya mambo makubwa
unayoyaona.
Wazo hutambuliwa kama chanzo cha utajiri, mawazo yenye mwanzo usio na faida sana yamekuwa chimbuko la matajiri wakubwa duniani.
Wazo linaweza kuzalisha pato
zaidi ya daktari, mwanasheria, mhandisi wakawaida kwasababu yeye itamchukua
muda mrefu kujifunza sana ndio apate anachotaka.
Maarifa sahihi yanaweza kuwa kitu
cha kuchochea wazo kuendelea mbele, picha juu ya nini anataka kufanya ndio inayoweza kupatanisha maarifa aliyonayo na wazo lake.
wazo huletwa na ubunifu, wazo
ndio kitu kikuu na maarifa hupatikana na kutumika baada ya uwepo wa wazo. Unaweza
usiwe na elimu kubwa ukapata wazo zuri baada ya kutumia ubunifu kupata picha
kubwa inayokuhusu.
Bila ya mawazo duniani tungekuwa
bado tupo zama zile za mawe. Mawazo yameathiri kwa sehemu kubwa maisha ya
wanadamu duniani na sipati kigugumizi kusema kuwa dunia inaongozwa na watu
waliokwisha kufa miaka mingi sana iliyopita. Ndio, waliokufa wengi mawazo yao
bado yapo yanaishi duniani, na yanatawala kila kona ya maendeleo tunayoyafanya
na mengine yametufunga hata tukashindwa kuwaza mambo mapya.
Kuanzia darasani, mtaani mpaka
uwanja wa siasa ni mawazo ya watu. Vip kuhusu imani je? Serikali, biashara na
mengine mengi? Utakuja kugundua hata imani ambazo leo watu wanauana kwasababu
ya hizo zilikuwa ni wazo tu na likapata kudhihirika na kuwa uhalisia.
Mungu ndio chanzo cha mawazo na
akatoa mfano kwa kuonesha wazo linatendekaje. Wazo lake limejificha kwenye neno
lake analotamka, maagano anayoweka na watu wake tangu mwanzo wa ulimwengu.
Mawazo yanatabia ya kuibuka na
kutoweka na kurudi tena upya kwa muonekano mwingine. Mungu akamuumba mwanadamu
na akampa kutawala dunia na vitu vyake vyote. Mwanadamu alipomkosea Mungu ,wazo
la Mungu alikuishia hapo liliendelea kujificha ndani ya maagano aliyoweka na
vizazi kama Ibrahim (mwanzo 12:1-3), Isaka (mwanzo 17:19), Yakobo ambaye ndio Israel
(mwanzo 28:13_22). Hii ni kukuonesha kuwa mawazo yanatabia ya kutoweka na
kuibuka huwa hayafi hata mtu akifa yanaendelea kuishi.
Wazo hilo la Mungu la kumpa
mwanadamu utawala halikufa licha ya vizazi hivyo kupotea. Vikapita vizazi 42
tangu ibrahimu ( mathayo 1) kupokea wazo hadi kuja kwa Messiah ( Yesu Kristo)
duniani kukomboa ulimwengu kwa mara ya kwanza na kufa msalabani kama wazo la
Mungu lilivyomtaka. Wazo lilifukiwa katika kipindi cha agano la kale na Mungu
hakulifanya siri akazidi kulifungua kwa manabii mbalimbali.
Wazo la Mungu linaishi hata leo
kwa wale wanaoamini ( hebrania 9:15) kwamaana Yesu kristo ndiye mbeba maono
yaliyotokana na wazo la Mungu hao watu wanaitwa wakristo yaani wapakwa mafuta.
Lengo langu halikuwa kueleza
imani, La, bali ni kukuonesha kuwa unatakiwa kuwa na wazo linaloweza
kukuzidi umri na kuishi zaidi yako vizazi na vizazi na kusaidia watu wengi.
Leo tunazungumzia demokrasia ambayo
ilikuwa wazo la wayunani wa athene lakini hadi leo wazo linaishi. Hata simu
unayotumia ilitokana na wazo la mtu Fulani ambaye wazo lake lilitokana na wazo
la mtu mwingine. Steve Jobs alileta mageuzi ya teknolojia ya mawasiliano ya
simu bila waya, lakini kabla yake kuna mtu anaitwa Martin Copper kabla ya
Copper alikuwepo Alexander Graham Bell.
alipokufa Galileo Galilei 1642 ndio mwaka ambao Isaac Newton alizaliwa na wote walitoa mchango mkubwa kwenye kanuni za fizikia hasa mwendo wa viumbe vya duniani na angani.
Siri kubwa ya mafanikio yetu ipo
kwenye mawazo yanayotokana na kufikiri kwetu kila siku, unawazo nini na
unafikiri nini? Wazo linatoka wapi? Na maswali mengine mengi yakujiuliza unatakiwa kuwa nayo.
unaweza kuamua dunia iweje kama unawazo lenye nguvu na ukalitendea kazi, kama tunavyoona leo mawazo mengi yakipita duniani kuamua maisha ya watu wengi huenda bila ridhaa yao. nimeandika dunia inaongozwa na watu waliokwisha kufa kwa maana ya kwamba waliacha mawazo makubwa yanayoendesha dunia.
Tuna watu wachache wenye mawazo makubwa wanaoishi leo nao pia wanaendesha dunia, ukiamua unaweza kuwa mmoja wao au ukawa mpokea mawazo na kuyatendea kazi vyovyote ni sawa.
Mungu ametupa fursa ya kuvumbua mawazo mapya tutumie uwezo wa ndani tulionao kujenga picha ya maisha tunayoyataka kuishi na wazo litakuja, kama ni la Mungu litasimama na kudumu na kuleta mageuzi duniani, vinginevyo litaangushwa.
Frank Mwakajila
mwandishi.
Comments