KANUNI 16 ZA KUISHI MAISHA YAKO.

rethink relive


Habari yako ndugu msomaji wangu, wa mfululizo wa machapisho yanayogusa maisha yetu moja kwa moja hususani uwezo tulionao wanadamu wa kutufanya tuishi. Maisha yanakila kitu tunachotaka ila maisha hayatupi tunachotaka bali hutupa tunachotafuta kwa kuanza na kunia kupata.
Leo tuangazie kona ya kuishi maisha yetu halisi, Tambua unawajibu wa kuishi maisha yako sio maisha ya mtu Fulani mashuhuri au mzazi wako. Maisha yetu yanaweza kutiwa hamasa na mtu ila sio kigezo cha kuishi kama yeye binafsi naita huo ni uvivu wa kufikiri.

Hizi ni kanuni kumi sita za kuishi maisha yako.

Penda kupenda.
Upendo ni hali  ya asili ila  inataka utayari wa mtu husika, katika upendo mambo mengi yanafanikiwa, upendo ni dawa sio ya homa bali ya maisha kwa ujumla. Ndio maana vitabu vya kiimani imesisitiza sana, na kikristo upendo ni Mungu, yani Mungu ndio pendo. Ukitaka kuishi maisha yako kuna upendo unatakiwa kuwa nao, ni ule unaotokana na Mungu yani unaweza  mpenda  mtu bila sababu ya kibinadamu. Ukimpenda hutaweza mwonea wivu, kumsengenya wala kufurahia akishindwa. Upendo ndio mzizi wa maisha yenye furaha duniani.
Ukifika mbali zaidi utaona upendo unaoanzia kwako mwenyewe yani kujipenda kujitendea haki mwenyewe kama anavyostahili binadamu. Umewahi kuona mtu anaambiwa "wewe hujipendi" ndio hutokea baadhi ya watu wabishi wasiojipenda. Kwasababu upendo ni chanzo cha yote tuendelee kuangalia kanuni nyingine zinazozaliwa na upendo.



Ishi kwa malengo
Kudumu tunadumu wengi duniani ila kuishi tunaishi wachache sana, inahitaji utoke kwenye hatua ya kudumu uanze kuishi ndio upange hayo malengo. Malengo, matazamio na maono ni maneno yanayokaribiana kimaana. Maisha mpaka yaitwe yako yanatakiwa kupangwa na wewe mwenyewe bila kuingiliwa. Naupenda ule msemo wa "naenda kuanza maisha" huyu mtu alikuwa anaishi maisha ya watu wengine kwa malengo waliyokuwa wamepanga hao watu, huenda ni wazazi,.
"Ubongo ni kiwanda cha maamuzi " napenda kusema hivyo, mawazo yako yakupelekee kufanya maamuzi juu ya malengo gani unayo katika safari hii ya maisha. Ikumbukwe kuwa maisha sio mbio za muda mfupi kwamba hata ukijikwaa hakuna shida bora ufike, maisha ni safari ndefu inayohitaji kufanya mambo. Ukiweka malengo usipo weka malengo ni juu yako ila lazima tufanye.

Jiheshimu heshima wengine.
Swala la kujiheshimu linaweza kuwa tata, kujiheshimu ni kufanya mambo yanayofanana na wewe unayetenda. Kuheshimu wengine ni kuwapa watu wengine stahiki zao kulingana na vigezo mbalimbali kigezo mama ni wao kuwa watu Kama wewe. Napata shida sana pale mtu anaposhindwa kuwianisha heshima kwa watu sababu ya mmoja wao kuwa zaidi kwenye maeneo Fulani, kama tajiri au jinsia fulani na wakati mwingine kabila.
Kuheshimu watu kutakufungulia njia ya kuishi maisha yako kwa namna ya pekee pale watu watakapo kutafsiri kwa mtazamo chanya na kuona thamani yako. Inanishangaza ninapopata muda kwaajili ya mtu alafu anakuwa hajari.

Kuwa na tabia ya shukrani
Hii ni tabia ya mrejesho wa kila ulichofanyiwa na huwezi kuonesha bila hata kutoa kitu kwa mtu husika. Ukiwa mtoto wanakuacha ila ukikua watakushangaa kama haushukuru. Ukishukuru unatengeneza mazingira ya kutokuwa ombaomba sababu watu watarudi kukupa vitu vyao wakijua wanatoa mahali sahihi. Kumshukuru Mungu pia ni ishara ya kujikubali vile ulivyofanyika kwa uwezo wa Mungu. Neno asante likitoka moyoni linaambatana na hisia ya maisha yako halisi, tathmini pale unapotoa shukrani kwa Mungu ama kwa mtu huwa unapata hisia gani. Furaha huweza kuja na machozi kuonesha hukutarajia yale uliyotendewa.

Kutoa
Mfano wa mwili kama mashine kila kitu kikiingia mwilini mabaki yake au ziada yake kutoka nje ya mwili kama haviitajiki, na kitu cha ajabu sana ni kwamba hivyo vitu vikitoka nje hutumika kwa namna nyingine ya asili. Kama maisha ni kujifunza basi mada ya kwanza iwe kutoa. Yote uliyonayo umepata kwa waliokuzunguka, deni kubwa ulilonalo ni kurudisha vyote walivyokupa. Utapoona kutoa ni kupoteza kwasababu ya kukimbizana kimaendeleo na fulani, hakika utatumia nguvu nyingi pasipo ulazima.

Kuwa na muda na rafiki na familia yako.
Ni kweli kuwa kuna vitu hawawezi kukupa hasa vile unavyopambana kuvifanya kulingana na malengo yako, ila ni msingi mkubwa wa maisha yako, rafiki na ndugu wa familia. Kuna mambo yako utataka kuwauliza kuna tatizo ulilonalo hao ni wa kwanza." Waswahili wanasema rafiki wa kweli ni mama na baba"

Tambua thamani yako
Kuna wakati unafika mpaka unagombana na mtu sababu ya yeye kutokufahamu thamani yake. Kuishi chini au juu ya thamani yako hupelekea kuishi nje ya maisha yako. Kuna msemo mmoja wa mama simba anamwambia mwanae kuwa mwanangu hata kama mawindo hayapo usile majani bora ufe njaa. Thamani yako itakuongoza kufanya vitu aina  Fulani, kukaa na watu wa sina fulani , kuwepo mahali fulani.

Tafuta fursa za kujifunza
Maisha yanahitaji ujuzi mbalimbali hivyo fursa za kujifunza ni za kutafutwa , wengi hatupo tayari kujifunza vitu vipya na kutufanya tuishi maisha yaliyochukuliwa kwa watu wengine yaani kukopi.

Tambua uwezo wako
Kila kiumbe ameumbika akiwa na uwezo wake wa ndani, ndio maana wako vilema,vipofu na walemavu wengi mashuhuri duniani waliofanikiwa kupitia sehemu ya maisha yao iliyokuwa sio dhaifu. Uwezo hututofautisha na kutuongoza njia ya kutupeleka kwenye maisha yetu sahihi. Unachokiona Leo duniani ni uwezo wa watu uliojidhihirisha nje. Wewe halisi sio unayeonekana ni yule aliye ndani yako ambae anaendelea kujidhihirisha. kazi kwako kutumia uwezo wako.


Kuwa halisi
Maisha sio maigizo ni uhalisia, weka malengo halisi, mpango halo halisi, mikakati halisi. Wewe unajifahamu uwezo wako na yale yanayowezekana katika hali uliyonayo. Nashangaa pale mtu anapofanya kitu ambacho hajawahi kuliwekea mpango na kupima uwezekeno wake, usinielewe vibaya, kuna tofauti kati ya kufanya tu na kunia kufanya. Hana nia, mpango, mkakati wa jambo alafu unalifanya.

Rahisisha mahitaji yako.
Unapata kiasi gani, unatumia kiasi gani. Tambua vitu unavyohitaji, uwe na vipaumbele vyako achana na vipaumbele vilivyopendekezwa na watu. Mitindo mipya inapokuja sio kosa kuendana nayo ila ipo katika mahitaji yako? Unaporahisisha mahitaji yako unapata furaha maishani mwako kwa kuto sukumwa na halaiki ya watu wanataka nini.

Usijifananishe nao
Chanzo cha watu wengi kutoishi maisha yao ni kujifananisha na watu. Kumkubali mtu alivyo sio chanzo cha wewe uwe kama yeye. Chora njia yako pita mapito yako kunywa kikombe chako jenga hemaya yako. Umepewa kumfahamu huyo unayemuiga ili akuhamasishe kufanya makubwa katika maisha yako, sio kumuiga. Wengine ukijifananisha nao watakuvunja moyo kwa historia zao za kutisha kwa sababu mpaka wamefika hapo wamepitia mengi, watakufanya uendelee kuwa shabiki wao, hakuna aliyeumbwa duniani kuwa shabiki wa mwenzake.

Jikubali
Watu wengi hawajikubali kwasababu ya kugundua udhaifu walionao kabla ya kugundua uwezo walionao. Tatizo linabaki palepale kwamba udhaifu ulionao unatabaki kuwa udhaifu kama utajifananisha na watu wengine, uwezo wako unaweza kukupeleka pale ambapo haujawahi kufika.

Jifunze kujisamehe na kusamehe wengine
Kuna maneno matatu yanataka kufanana, samahani, nisamehe na naomba unisamehe. Naomba unisamehe linajieleza vizuri, linaonesha mwanzo mpya wa maisha yako na yule unayeomba msamaha kwake. Msamaha unaleta amani, huenda ulikuwa unaishi maisha yako vizuri kwa kushirikiana na rafiki ila ghafla mkakwazana, bila ya kuomba msamaha unaendelea kukosa yale uliyokuwa unapata kutoka kwa huyo rafiki yako.

Waza chanya
Una macho unaona, una masikio unasikia una hisia unahisi, vyote huja na hali tofauti tofauti kuwa tayari kuweka mtazamo chanya kwa kila jambo. Ndio wakati mwingine mambo yapo hasi kabisa ila kama unaishi maisha yako yaliyo hasi huweza kubadilika na kuwa chanya. Unaonaje jamii inayokuzunguka? Unaonaje elimu yako? Unaonaje mshahara wako au biashara yako?? Na una tamka nini??
Watu chanya hufanikiwa sana kwa sababu ya kugundua maisha yao. Ukiwa makini utagundua kuwa unachokiwaza Mara nyingi hutokea. Wakati mwingine huwa hatupati mishangao (surprise) sababu tunakuwa tumewaza yaleyale yatakayotokea na yanatokea.

Andika nakala ya maisha yako
Unaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kusahau, ni jambo zuri kuandika nakala yako kuhusu maono na mikakati ya kutimiza hayo maono uliyonayo. Pamoja na kuandika nukuu zako muhimu kukusaidia kukaa kwenye mstari uliyonyooka kwenye safari hii ya maisha. Huwa nikipitia nakala zangu zinazohusu maisha yangu huwa napata nguvu ya kusonga mbele.

Palipo na upendo kuna maisha palipo na maisha kuna mafanikio, mtu  asikutishe kuwa ukifanya hivyo unavyofanya sio sahihi, pata ushauri kwa mtu sahihi wakati mwingine mtu sahihi ni wewe mwenyewe. Mtu mwenye mawazo hasi Mara zote hatoi suluhu ya tatizo bali  atakuongezea tatizo.

Kazi ni yako ya kuasimama na uamuzi unaoona ni sahihi kwako. Mungu atusaidie kuishi maisha yetu aliyotupangia.

Na;-
Mwalimu Mwakajila Frank. A, Jr
C.E.O
World Inspiration Inc
Inspired by God of ðŸ‡¹ðŸ‡¿ðŸ‡®ðŸ‡±

Comments

Popular posts from this blog

MWANAMKE WA THAMANI NA TABIA ZAKE 30

KUJIKATAA.KUKATALIWA.KUKATA TAMAA.

UNAWEZAJE KUKOMBOA WAKATI